Mimi kama Mkenya nimechoshwa na Wabunge wetu wanavokiua Kiswahili katika Bunge. Ningeomba Serikali iwalipie somo hili ili waache kutuaibisha au ikomeshe upeperushaji wa moja kwa moja, au hata wa baadaye wa vipindi ambavyo vinatuaibisha kama nchi. Kenya ni nchi moja ijulikanayo kwa lugha hii tuipendayo lakini ukifika huku nchini unapata asilimia ndogo sana yakijua. Jiulize watu wa nje hujiulizaje wanaposikia Wakenya walivo wataalamu kwa lugha ya Kiingereza wakati lugha yao ya taifa hawaijui. Najua kwamba umuhimu wa mazungumzo au mawasiliano ni kuelewana ('bora tuelewane') lakini angalia jinsi nchi kama Uingereza zinalinda lugha zao. Cha kushangaza ni kuwa Makao ya Bunge yanaonyeshwa moja kwa moja kwenye runinga zetu na Wabunge wasiokijua, Mwenyezi Mungu awasaidie, ndio wanakimbia kukizungumza. Wabunge wetu mwatukera! Kiswahili ni lugha ya taifa nchini Kenya lakini mwajifanya kutokijua, na wengine wenu hamjifanyi kwani hamkijui ng'o! Kunao ambao wanafurahia kukiporomosha Kiingereza ili kuwaacha watazamaji na wabunge wenzao na mshangao lakini kwani hamjui kwamba mwacha mila ni mtumwa? (charity begins at home). Wabunge wanafaa kutozwa faini kubwa wakikosea Kiswahili. Spika Maalim anafaa apelekwe shuleni. Waziri Mkuu pamoja na rais, nyie twawapenda lakini tafadhali acheni kukiua Kiswahili. Rais Kenyatta alikipenda Kiswahili na ndio maana Wakenya wa siku zile hawakuongea jinsi tunavoongea. Wasanii wa siku zile waliimba kwa Kiswahili kitamu. Mtu akifanya kosa katika Kiswahili twacheka sana, ilhali akikosea neno moja tu la Kiingereza twamshangaa kweli. Huu, kama anavouliza Mbotela, ni uungwana? Eti heri kumpenda mtu mliyekutana hivi majuzi, kuliko wa familia yenu. Huu ni upumbavu. Nikirudi kwa Wabunge, wasiokijua Kiswahili wanafaa watimuliwe, na upumbavu wanaouita Sheng unafaa uzikwe katika kaburi la sahau. Kiswahili ni mama na baba. Kiingereza ni jirani tu!
Nina ombi moja tu kwa Wabunge wetu: Kama hamkijui Kiswahili jifunzeni kabla ya kujiabisha mbele yetu. KBC na nyumba zingine za utangazaji zapeperusha duniani kote. Mtakosa kura zetu kwa sababu hiyo tu!
No comments:
Post a Comment
What do you think about it?